Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hassan Fadlullah, mbunge wa Kundi la “Uaminifu kwa Muqawama”, katika hotuba yake kwenye hafla iliyoandaliwa na Hizbullah kwa mnasaba wa kuzaliwa kwa Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) katika Majmu‘a Imam Kadhim (amani iwe juu yake) kwenye eneo la Madi, alisisitiza kuwa nguvu ya muqawama nchini Lebanon hutokana na nguvu ya watu wetu. Sote tulisikia sauti ya kitaifa na ya muqawama iliyotoka kwa watu wa Kusini, wale ambao mali zao zilivamiwa. Sauti hiyo pia tuliisikia kutoka katika familia za mashahidi — baba, mama, wake na watoto — msimamo unaounga mkono na kutetea muqawama. Kwa msingi huu, hakuna nguvu yoyote nchini Lebanon inayoweza kung’oa muqawama kutoka miongoni mwa watu hawa, wala hakuna nguvu yoyote duniani inayoweza kuwatenganisha watu hawa na ardhi na nchi yao.
Alisisitiza kuwa; licha ya ukatili wa mashambulizi, udhaifu wa serikali na vyombo vya utawala nchini Lebanon na ushirikiano wa baadhi ya watu, umma huu ulio huru, jasiri na wenye kujitolea ni watu wanaoweza kusimama dhidi ya jaribio lolote la kung’olewa kutoka katika ardhi yao; hakuna mtu atakayeweza kuwafukuza kutoka Kusini.
Fadlullah alisema kuwa; kwa kutegemea watu hawa wema — wanaume, wanawake na watoto waliosimama imara na kuyakabili mauti — pamoja na subira, ustahimilivu, kujitolea na irada ya watoto wetu miongoni mwa wapiganaji jasiri, watapita katika hatua hii ngumu na kuelekea mustakabali bora. Nyakati ngumu hazitawazamisha wala kuwavunja moyo, kwa sababu wanashikamana na matumaini ya madrasa ya Mtume Mtukufu (rehema na amani zimshukie yeye na Aali zake) na kiongozi wake wa leo, Imam Mahdi (a.f.). Wafuasi wa madrasa hii daima wameinuka dhidi ya dhulma; Mashia katika historia yote wamebeba bendera ya kupambana na madhalimu, na leo wako mstari wa mbele kupambana na ukaliaji, dhulma, uvamizi na kiburi cha adui; kizazi baada ya kizazi kinatoa gharama na kujitolea.
Mjumbe huyo wa Kundi la Muqawama aliongeza kuwa; wanakabiliana na matatizo wanazuoni wao na viongozi wao — kuanzia Maimamu hadi marjaa na makamanda — huuawa kishahidi, na hili ni sehemu ya madrasa yao. Katika kipindi hiki pia, Sayyid na kiongozi wao Sayyid Hassan Nasrullah aliuawa kishahidi katika njia ya jukumu hilo la Kiungu la kubeba bendera hiyo. Historia yao imejaa nyakati kama hizi, lakini bendera itaendelea kubaki juu na kulindwa.
Fadlullah aliwahutubia wafuasi wa muqawama akisema: Msihofu mustakabali na msisikilize kelele zote za ndani; hakuna kati ya hayo yenye athari. Kilicho muhimu ni kusimama imara mbele ya mienendo ya nje — hasa mashambulizi yanayotulenga. Kama walivyoshindwa mwaka 1982, watashindwa pia katika siku zijazo, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na tutabaki katika nchi hii; hakuna tufani itakayoweza kututikisa.
Aliendelea kusema kuwa; wanapita katika hatua mpya na hawakanushi kuwa changamoto na matatizo ni mengi. Licha ya maumivu, majeraha, misiba na damu ya thamani inayomwagika kila siku, wanaitaka serikali ichukue majukumu yake. Ingawa baadhi huuliza ni serikali ipi inayokusudiwa, bado ina wajibu kwa wananchi wake na inapaswa kutekeleza majukumu yake.
Fadlullah aliongeza kuwa; katika muktadha huu kuna uzembe, udhaifu, kuchelewa na wakati mwingine maelewano kutoka kwa baadhi ya maafisa, lakini bado wanasisitiza serikali itekeleze wajibu wake. Katika vikao vya baraza la mawaziri, bunge na mawasiliano ya kila siku na maafisa, wanaendelea kuwataka wachukue msimamo wa kitaifa kuhusu yanayoendelea. Wananchi wameona tofauti ya wazi kati ya vipindi viwili: wakati muqawama ulikuwa na nafasi yake, adui hakuthubutu kufanya uvamizi wowote dhidi ya nchi au hata kukaribia mipaka; lakini pale jukumu la kulinda ardhi lilipowekwa mikononi mwa serikali pekee, hali ilibadilika.
Alikumbusha kuwa; mwaka 2024 walikabiliana na uvamizi wa Israel, walipigana, vijana wao waliuawa kishahidi katika mipaka na hawakumruhusu adui kuikalia ardhi. Walikabidhi eneo la Kusini lililo nje ya mto Litani kwa serikali ili itekeleze mamlaka yake juu ya ardhi iliyosafishwa kwa damu ya mashahidi, lakini serikali ilipokuja kutekeleza hilo, adui alizidi kuwa jasiri na watu hawakuona msaada wowote kutoka kwa serikali; hali iliyoongeza pengo kati ya wananchi na serikali.
Fadlullah alisisitiza kuwa; wao ni sehemu muhimu ya serikali nchini Lebanon; ni washirika wa kweli wake na watalinda ushirika huo. Watailazimisha serikali kutekeleza majukumu yake kwa njia yoyote. Aliwaambia maafisa kuwa kuna misingi minne inayopaswa kufanyiwa kazi:
1. Kuondoka kwa adui katika ardhi zinazokaliwa.
2. Kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel.
3. Kuachiliwa wafungwa.
4. Kujengwa upya maeneo yaliyoharibiwa.
Alisema pia; hadi misingi hii itakapotimizwa, hakuna hatua nyingine ya ziada inayoweza kujadiliwa. Leo damu ya wapendwa wao inaendelea kumwagika Kusini na maeneo mengine, mashambulizi yanaendelea na ukaliaji bado upo; maadamu uvamizi unaendelea, hakuna mazungumzo kuhusu jambo jingine.
Aliongeza kuwa; baadhi ya pande zilipendekeza kupelekwa kwa jeshi Kusini mwa Litani na kutekelezwa kwa Azimio 1701 pamoja na makubaliano ya kusitisha vita, na wao walikubali kwa ajili ya maslahi ya nchi na watu wao, kwa sababu hawataki vita vipya na si wao walioanzisha vita; bali adui ndiye aliyelazimisha. Hata hivyo, adui huyo baada ya kila hatua ya upendeleo huomba zaidi bila wadhamini wa kimataifa kutoa dhamana yoyote.
Mwisho, Hassan Fadlalluh alisisitiza kuwa; uhuru wa nchi (sovereignty) si jambo la kufanyiwa majaribio, na kuilinda si suala la majadiliano au ujanja wa kisiasa. Kila aliye katika nafasi ya uongozi anapaswa kubeba wajibu huo wa kitaifa. Katika kipindi hiki wanapaswa kuwa na subira na ustahimilivu; damu yao si ya bure, na vijana wao mashahidi ni watoto bora na wapendwa wa taifa hili. Pamoja na mateso yote, bado wana matumaini ya mustakabali, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Maoni yako